Thursday, May 21, 2015

0
PICHA 21 ZA VURUGU NJOMBE KATI YA WANANCHI NA POLISI ZIANGALIE HAPA

.Sababu ni kile kinachodaiwa askari polisi kumuuwa kwa risasi mwananchi wa mtaa wa kambalage na kumjeruhi mwingine

 kijana Basil Ngole Anayedaiwa kuuawa na polisi jana usiku majira ya Tatu Huko Kambalage Njombe Kijana Fredy Ambaye Alijeruhiwa Akiwa Hospittal ya Mkoa wa Njombe Huko Kibena Asubuhi ya Leo
 
 

0
NEWZ ALERT:WALEMAVU WAFUNGA BARABARA KARUME-ILALA JIJINI DAR LEO, PICHA ZIKO HAPA

 Umati wa watu ukionekana katika eneo la Makutano ya Barabara ya Kawawa na Uhuru, Karume jijini Dar es salaam kutokana na kuwepo kwa baadhi ya walemavu wa viungo waliokaa katikati ya Barabara hizo kushinikiza kupewa eneo la Karume ili waweze kufanya biashara zao, hali iliyopelekea njia hizo kufungwa kwa muda na kuleta usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo.PICHA KWA MUJIBU WA MICHUZI MEDIA GROUP

0
MAMA AMUUZA MWANAYE SHILINGI 70,000 HUKO MONDULI.....KISA MAISHA MAGUMU

Mkazi mmoja wa Kijiji cha Nanja, Kata ya Lepruko, wilayani Monduli, anadaiwa kumuuza mtoto wake wa kumzaa kwa mtu mwingine kwa Sh70,000 kwa madai kuwa ana maisha magumu.
Katika tukio hilo la kushangaza, inadaiwa mwanamke huyo aliamua kumuuza mtoto huyo wa kiume mwenye umri wa miezi minane katikati ya Mei, mwaka huu akiwa ametoka naye mkoani Singida.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nanja, Time Samsoni akizungumza juzi mbele ya Mratibu wa Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA) Tawi la Arusha, Francisca Gaspar alisema walijaribu kumshawishi akamchukue mtoto wake, lakini aligoma.
Mwenyekiti Samsoni alidai kuwa mtu aliyemnunua mtoto huyo anaishi katika Kijiji cha Longonito na ana wadhifa mkubwa kijijini hapo.
“Kwa kweli tulisikitishwa na kitendo hicho cha huyo mwanamke kumuuza mtoto wake kwa Sh 70,000 akisingizia maisha magumu na ameshindwa kumlea,” Samsoni.
Alisema walimwita mwanamke huyo kwenye ofisi ya kitongoji na kumhoji sababu zilizomfanya amuuze mwanaye, lakini aliwaaambia kuwa hana uwezo wa kumhudumia.
Mratibu wa Tawla, Gaspar alisema watahakikisha wanafuatilia suala hilo ili lipatiwe mwafaka. “Lakini tumeambiwa kuwa mama huyo ametoroka baada ya kuhojiwa na viongozi wa hapa kijijini na hajulikani aliko mpaka sasa.”

CHANZO: MWANANCHI

0
MMOJA AFARIKI DUNIA WAKATI AKIWA KWENYE FOLENI YA KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGAKURA

Mtu mmoja amefariki dunia baada ya kuanguka ghafla akiwa kwenye foleni ya kwenda kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa teknolojia mpya yaBiometric Voters Registration (BVR).
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi saa 6:30 mchana kwenye kituo cha Lusyoto, kata ya Mpuguso katika eneo la Ushirika, wilayani Rungwe, ikiwa ni siku ya kwanza ya kuanza uandikishaji wa wapigakura wilayani humo.
Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo wamemtaja aliyepoteza maisha kwenye tukio hilo kuwa ni Mary Kabejela anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 60, mkazi wa Ushirika wilayani Rungwe.
Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya mashuhuda walisema Mary akiwa kwenye mstari wa foleni ya kuelekea kwenye chumba cha uandikishaji, ghafla alionyesha kudhoofika na kuishiwa nguvu na kisha kudondoka chini.
Amani Mwaipaya, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema baada ya mama huyo kuanguka, wananchi walimwinua na kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Rungwe ya Makandana, ambako alipoteza maisha wakati akipatiwa matibabu.
“Tulimwona akianza kulegea na ghafla akaanguka chini, ndipo tulipomwinua na kumpakia kwenye gari tukampeleka hospitali, lakini wakati daktari akianza kumhudumia alifariki dunia,” Mwaipaya.
Baadhi ya wananchi na viongozi wa kisiasa waliozungumzia tukio hilo, walisema kifo cha mama huyo huwenda pia kimechangiwa na kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu kutokana na kasi ndogo ya uandikishaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahamed Msangi, hakupatikana kuthibitisha tukio hilo licha ya simu yake ya mkononi kuita kwa muda mrefu.
Mwandishi wa habari hizi alifika kwenye ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya na kuelezwa kuwa Kamanda Msangi amesafiri kikazi na kwamba kaimu wake, Nyigesa Wankyo pia alikuwa nje ya ofisi kikazi.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Mbeya Mjini,David Mwambigija, maarufu kwa jina la Mzee wa Upako, ambaye yupo wilayani Rungwe kama wakala wa chama chake kwenye kazi hiyo, alisema uandikishaji unafanyika kwa kasi ndogo, hali inayosababisha watu kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu na hata kusababisha presha kuwapanda.
“Inawezekana huyu mama akawa amekufa kutokana na presha kupanda, kwani alisimama kwenye foleni tangu asubuhi huku akipigwa na jua kali, kutokana na umri wake kuwa mkubwa huenda presha ilimpanda na kumpelekea kupoteza maisha,” alisema Mwambigija.
Alisema kasi ya uandikishaji siyo nzuri kutokana na watumishi wa serikali waliopewa kazi hiyo kuonekana kama wanajifunza hivyo kutumia muda mrefu kukamilisha kumwandikisha mtu mmoja, hali inayosababisha watu kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu.
Mbali na tukio hilo la kifo, zoezi la uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura  lilianza juzi kwa kusuasua wilayani Rungwe kutokana na madai kwamba mtandao ulikuwa na matatizo.
Kufuatia mtandao kuwa siyo mzuri, idadi kubwa ya vituo vya kuandikishia wapigakura vilichelewa kuanza uandikishaji hadi saa 4:00 asubuhi hali ilipoanza kutengemaa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Veronica Kessy, alikiri kuwapo kwa changamoto katika siku ya kwanza ya uandikishaji, ikiwamo tatizo la mtandao kusumbua.
Alisema hata hivyo tatizo hilo lilikuwa la muda mfupi na baadaye hali ilikuwa nzuri na kasi ya uandikishaji ikaendelea vizuri kama lilivyopangwa katika maeneo mengi.
Kessy alisema ni vituo vichache tu ambavyo zoezi la uandikishwaji wapigakura liliingia dosari kwa kukumbwa na changamoto ndogondogo kama vile kuchelewa kufunguliwa, kujitokeza kwa idadi kubwa ya wananchi kuliko uwezo wa waandikishaji na tatizo la mtandao kusuasua.
Katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya zoezi la uandikishwaji lilianza juzi katika kata 10 zilizopo ndani ya Bonde la Uyole, ambako liliendelea vizuri licha ya wananchi kulalamikia kasi ndogo ya waandikishaji.
Katika kituo cha Isyesye kulitaka kutokea tafrani baada ya wananchi kumshtukia mtu mmoja anayedaiwa kuwa kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukaa pembeni mwa kituo cha kuandikishia wapiga kura akiwa na daftari na kalamu akiorodhesha watu wanaojiandikisha.
Wananchi hao walimjia juu mtu huyo wakitaka kumpiga kabla ya askari wa Jeshi la Polisi kuingilia kati na kumwondoa kwenye eneo hilo kabla hajaanza kushushiwa kipigo.
Awamu ya tatu ya uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ilianza jana mkoani Dodoma na Tabora utaanza leo, huku Katavi ukiwa umeanza tangu Jumatatu iliyopita.
Awamu ya kwanza ilihusisha mkoa wa Njombe ambayo ulikamilika katikati ya Aprili, wakati awamu ya pili inaendelea katika mikoa ya Ruvuma, Iringa, Lindi na Mtwara.
Uandikishaji huo umekuwa ukilalamikiwa kusuasua kutokana na kasoro kadhaa hususani uchache wa vifaa (BVR kit), uchache wa waandikishaji na  vifaa hivyo mara nyingi kukwama kufanya kazi.

0
WANANCHI WA NJOMBE WAPATA WAKATI MGUMU BAADA YA MAMBOMU YA POLISI KURINDIMA

Wakazi wa Mji wa Njombe, jana walikumbwa na taharuki kutokana na mabomu ya machozi yaliyopigwa na Polisi kwa lengo la kutawanya waandamanaji waliokuwa wanapinga mauaji ya mkazi mmoja anayedaiwa kupigwa risasi na askari na mwingine kujeruhiwa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Franco Kibona alisema jana kuwa hawezi kuzungumzia tuhuma hizo wakati hali ya kiusalama haijatulia.
Kamanda Kibona aliyekuwa eneo la tukio, aliwasihi wananchi kutulia kwani madai yao yanashughulikiwa.
Mauaji hayo yaliyotokea juzi usiku wakati wakazi hao wawili walipokuwa kwenye klabu ya pombe ya Nyondo, Mtaa wa Kambarage.
Wakazi wa eneo hilo walisema kuwa aliyeuawa ni Basil Ngole na majeruhi ni Fred Sanga ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Njombe.
Wakazi hao walikusanyika hospitalini hapo saa moja asubuhi, huku wakipaza sauti za kulitaka Jeshi la Polisi kugharamia mazishi ya marehemu pamoja na matibabu ya majeruhi.
Kutokana na kadhia hiyo, polisi walifika eneo la tukio na kuwatawanya waandamanaji kwa mabomu na kusababisha mmoja ambaye ni dereva wa bodaboda kujeruhiwa.
Kitendo hicho kiliamsha hasira kwa wananchi ambao waliziba barabara, kwa mawe, na kuchoma magurudumu ya gari.
Majeruhi Sanga akizungumza kwa tabu akiwa hospitalini alisema wakati akiwa katika klabu hiyo, askari wa doria ambao walikuwa hawajavaa sare walifika eneo hilo na kuwaweka wateja chini ya ulinzi.
Alisema hali hiyo ilizua mzozo, ndipo walipolazimika kufyatua risasi ambazo zilimpata yeye na mwenzake aliyefariki dunia.
Mkazi mmoja wa Njombe, Emanuel Filangali alisema kitendo cha baadhi ya polisi kutumia nguvu dhidi ya raia ni cha kulaaniwa.
Alisema kuwa inadaiwa kosa la marehemu na majeruhi ni kunywa pombe nje ya muda katika klabu hiyo.

0
MBUNGE ATAKA MKUU WAKE WA WILAYA NA MKURUGENZI WA HALMASHAURI WAJIUZULU HARAKA

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini amewajia juu Mkuu wa Wilaya ya Rombo,Lembrise Kipuyo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya hiyo, Anthony Tesha akiwataka wajiuzulu nyadhifa zao kwa kushindwa kusimamia sheria wilayani humo.
Selasini alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumzia taarifa ya wanawake wa Rombo inayodai kwamba wanakodi wanaume kutoka Kenya ili wafanye nao tendo la ndoa.
Juzi, gazeti hili liliripoti habari iliyomkariri Mkuu wa Wilaya kuwa baadhi ya wanawake wilayani humo, hukodi wanaume kutoka Kenya kwa ajili ya kufanya nao tendo la ndoa baada ya waume zao kupoteza nguvu kutokana na ulevi.
Eneo ambalo limeathirika zaidi na unywaji wa pombe haramu na zinazotengenezwa kiholela bila viwango ni la Kikelelwa lililopo mpakani mwa Kenya na Tanzania.
Taarifa hiyo ilimnukuu Kipuyo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo na kuitaja Kikelelwa kama eneo linalohitaji kutazamwa kwa jicho la pekee.
“Imefikia mahali wanaume wengi wanashindwa kumudu kufanya tendo la ndoa na kuwalazimu wanawake wao kukodi wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya tendo hilo,”  Kipuyo.
Kauli hiyo iliungwa mkono na baadhi ya wanawake waliozungumza mbele ya mkuu huyo wa wilaya katika operesheni ya kukamata pombe haramu ya gongo kijijini hapo iliyofanyika wiki mbili zilizopita.
Jana, Selasini alikanusha vikali taarifa hizo akidai kuwa siyo sahihi kuwajumuisha wanaume wote wa jimbo lake na ulevi huo au wanawake wote.
“Hiyo kauli haina utafiti wala haijaonyesha ni wanaume wangapi Rombo wana tatizo hilo au ni wanawake wangapi waume zao wana shida hiyo. Siyo sahihi kutoa kauli ya jumla,” .

0
WASICHANA WAWILI WAGOMA KUBOMOA NYUMBA ZAO ZILIZOJENGWA BARABARANI

1
Hii ni May 16 2015 ambapo kwa mujibu wa Wajenzi wa barabara, mmiliki wa nyumba hii anaendelea kuishi hapa japokuwa barabara imeshakamilika.
Hii ipo hata Tanzania unakuta barabara inabidi ipanuliwe so kuna watu tu watabomolewa nyumba zao ambazo ziko ndani ya eneo ambako ujenzi inabidi ufanyike.
Kwenye hizi picha za leo ni kutoka China ambako wamiliki wake wamekataa pesa zilizotolewa na idara ya ujenzi wa barabara kama fidia,
2
Picha ya April 2010 huko Guangxi Province
3
Hii nyumba wamiliki wake ni wazee Luo (67) na mke wake mwenye miaka 65 ambao waliingia kwenye mvutano na serikali kwa miaka minne kuhusu malipo yao na kuhama hapa.
4
Hata hivyo Luo alikubaliana na serikali na akalipwa zaidi ya MILIONI 80 za Kitanzania ndio akakubali kuhama na nyumba ikabomolewa December 2012.
5Hata hivyo wakazi wengine waliogomea nyumba zao zibomolewe baadae baadhi yao waliripotiwa kulipwa kiasi kikubwa cha pesa na kukubali kuondoka kupisha ujenzi.
6
7
8
9
10

0
MAMA AMFUNGISHA BINTI YAKE WA MIAKA 16 NDOA YA MKEKA

msichana mmoja anadaiwa kuwa na uhusiano na kijana wa kiume, lakini umri wake ni mdogo chini ya miaka 16.
Mama wa msichana huyo amesema mara nyingi amemzuia msichana huyo kutoingia kwenye chumba cha vijana hao lakini hasikii.. na siku nyingine huwa anatoka usiku kwenda kwenye chumba cha vijana hao.
Kijana wa kiume amesimulia jinsi ambavyo ilikuwa, amesema hana uhusiano wowote na msichana huyo ila mama wa msichana huyo aliwakuta wamekaa nje wanapiga story, akatishia kumwozesha ndoa ya mkeka.
Vijana wanaoishi chumba hicho wamesema kati yao hakuna hata mmoja ambae ana uhusiano na msichana huyo lakini msichana anapenda kuja kupiga nao story.

0
WEMA SEPETU ADAI "HATA MIMI NINGEKUWA AUNT EZEKIEL NINGEGOMBANA NA WEWE"

Staa wa filamu Bongo, Wema Sepetu.
Oscar ndauka
LICHA ya kupatana, habari ya mjini kwa sasa ni ugomvi mkali, wenye visa  vya kushangaza kati ya mastaa wawili wa sinema za Bongo, Wema Sepetu na Aunt Ezekiel.Hii ‘kapo’ siku za karibuni, ilikuwa nzuri kwa maana ya urafiki wao mkubwa.Urafiki wa Wema na Aunt ulianza pale Wema alipoutengua urafiki wake na staa mwingine wa fani hiyo, Kajala Masanja.
Wema Sepetu akiwa na Aunt Ezekiel.
Kuna visa lukuki kuhusu chanzo cha ugomvi wa Wema na Kajala, lakini ‘kuchukuliana’ bwana ndiyo kulitajwa sana!
Ikumbukwe kuwa, Kajala naye alirithi kijiti cha urafiki kwa Wema kutoka kwa msanii wa filamu na Mbongo Fleva, Snura Mushi.
TUREJEE KWA AUNT
Katika urafiki ambao ulionekana ungedumu zaidi ni kati ya Wema na Aunt kwa vile, Aunt alionekana kama mkomavu wa mambo ya ukaribu kuliko wengine, Snura na Kajala.Sasa siku za hivi karibuni, Magazeti Pendwa ya Global Publishers (ambayo huwa ya kwanza kufichua mambo ya siri ya mastaa), yaliandika kuhusu uhasama ulioibuka kati ya wawili hao chanzo kikiwa ni mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’.
Mpenzi wa sasa wa Diamond, Zarinah Hassan ‘Zari’ aliandaa shoo aliyoiita Zari All White Party iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar.
UGOMVI ULIANZA KWENYE PROMO
Inajulikana kwamba, mtu anapoandaa shoo, kikubwa ni kuipigia ‘debe’ kwa maana ya kwamba, watu wajue kuna shoo kubwa ili waweze kuhudhuria kwa wingi na ndiyo mafanikio ya mwenye kuandaa! Wakati shoo hiyo ikipigiwa debe na vyombo mbalimbali vya habari sambamba na wadhamini, Aunt aliandika ujumbe wa kuisifia, kwamba itakuwa ya nguvu na si ya kukosa, akaitupia kwenye mtandao wake wa Instagram.
AUNT MNAFIKI?
Habari zilimfikia Wema kwamba, Aunt ametupia kwenye ukurasa wake akiisifia shoo ya Zari All White. Hapo ndipo pakawa pabaya kwa Wema akitafsiri kwamba, kitendo hicho kwake ni kibaya kwa sababu Zari yupo na Diamond ambaye yeye alikuwa mpenzi wake zamani, akammwaga! Tena hapa ieleweke sawa, Wema ndiye aliyemmwaga Diamond.
Kumbe Wema anaishi na kinyongo cha Zari kwa sababu amemchukua ‘wa zamani’ wake, Diamond. Kwa hiyo ana bifu! Akitokea mtu akampa 5 Zari, kwa Wema mtu huyo anakuwa adui kama ilivyokuwa kwa Aunt Ezekiel ambaye ameonekana ni mnafiki! Anachekaje na Zari wakati Zari na yeye ni maadui?! (eti).
KWA NINI AUNT ALIFANYA VILE LAKINI?
Aunt alikuwa na kila sababu ya kuifagilia shoo ile kwa sababu moja kubwa sana! Ameshamwanika mpenzi wake wa sasa kwamba anaitwa Moses Iyobo! Huyu dogo ni dansa kwenye kundi la Diamond. Kwa hiyo shoo za Zari ilitegemea sana madansa wa Diamond.
Hivyo, Aunt alitumia nafasi hiyo kuwataka watu wafike kwa wingi, ukumbi ujae kutokana na kiingilio na waonesha shoo, akiwemo Iyobo walipwe vizuri, ili maisha yake na Aunt ambaye kwa sasa ni mjamzito, yaendelee. Sasa Wema alitakaje? Aunt aseme; ‘msiende shoo ya Zari, itakuwa mbaya sana’! Halafu ‘mzee’ (Iyobo) aende kula za uso? Ni akili kweli?
HUU NI UTOTO!
Mimi nauona huu ni utoto uliopitiliza! Katika hilo la Wema kumwona Aunt ni msaliti au mnafiki, hata mimi kama ningekuwa Aunt ningegombana na Wema na wala moyoni nisingeona nimepoteza chochote!
AUNT NA IYOBO
Naamini Aunt na Iyobo bado wapo sana kimaisha kuliko Aunt na Wema. Mbaya zaidi ukizingatia Wema mwenyewe kila rafiki anayempata anampoteza kwa uadui! Maana yake nini sasa!
Mimi namshauri (Wema) akae chini na kutafakari kwa mapana mwenyewe, na si kwa kushauriwa na akina Petit Man au Martin Kadinda, ajiulize ni kwa nini yeye! Na si kujiuliza ni kwa nini marafiki zake wengi humaliza nao vibaya!
Anaweza kuamini ana nuksi kumbe si nuksi bali ni maisha ya ubinafsi! Cha kwake anataka akiendeshe yeye na cha wenzake pia anataka akiendeshe yeye, hayo si maisha Wema bwana! Chenji!

CHANZO: GPL

0
CHADEMA YASIKITISHWA NA TAARIFA ZA UFISADI KATIKA UKAGUZI WA FEDHA ZA SERIKALI 2013/2014

  • Upotevu wa shilingi trilioni 1.151 Serikali kuu pekee hauvumiliki.
  • Makusanyo yote yaliyotokana na kuongezeka kwa kodi 2013/14 yameyeyuka
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ufisadi wa kutisha uliofanyika kwenye matumizi ya fedha za umma kama ilivyobainishwa kwenye ripoti za ukaguzi wa fedha kwa mwaka 2013/2014 zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
Wakati chama kinaendelea kuzifanyia uchambuzi wa kina ripoti zote tano ili kuweka hadharani ubadhirifu mkubwa ambao mwingi hujificha kwenye maelezo ya kitaalam, tunapenda kutoa taarifa ya awali kama ifuatavyo;
· Wizara tatu , Trilioni 1.151 zimepoteaKatika uchambuzi wetu wa awali tumebaini kuwa kwa upande wa serikali kuu pekee zaidi ya shilingi trilioni 1.151 zimepotea au kuliwa na wajanja walioko serikalini , kiwangio hiki ni sawa na asilimia 5.231 ya bajeti yote ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha 2015/16 inayoendelea kujadiliwa huko Bungeni Dodoma.
Ripoti ya CAG iliyotolewa jana inaonyesha kuwa katika Serikali Kuu, Wizara tatu tu ambazo tumezifanyia Uchambuzi mpaka sasa zimepotea kiasi cha shilingi 1.151 Trilioni , wizara hizo ni;
i. Wizara ya Fedha (TRA) , Fedha zilizopotea kutokana na bidhaa ambazo zilipaswa kuuzwa nje ya Nchi ila kutokana na uzembe zikauzwa ndani ya nchi bila kulipiwa kodi zilikuwa jumla ya shilingi 836 Bilioni.
ii. Ofisi ya Waziri Mkuu , kitengo kimoja cha maafa zilipotea jumla ya shilingi 163 Bilioni.
iii. Wizara ya Ujenzi , ziliibwa jumla ya shilingi 252 Bilioni.
· Bajeti ya mwaka 2013/14 Mapato yote ya ongezeko la kodi yameyeyuka:
Mwaka 2013/14 yalifanyika maboresho ya sheria mbalimbali za kodi wakati wa Bunge la bajeti kodi ambazo kimsingi zilimwongezea mwananchi mzigo mzito wa kulipia kodi hizo kwa ajili ya kuongeza mapato ya Serikali na ili kuiwezesha serikali kuwahudumia wananchi wake .
Pamoja na ongezeko hilo la kodi ,ukweli mchungu ni kuwa fedha yote iliyokusanywa kutokana na ongezeko la kodi mbalimbali katika mwaka wa fedha 2013/14 imepotea yote katika wizara tatu tu za serikali kutokana na vitendo vya kifisadi, na hii ni kwa mujibu wa taarifa CAG .
Kodi zilizorekebishwa na mapato yake ni kama ifuatavyo;
a. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148; kilipatikana kiasi cha sh.48.977bilioni
b. Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332;kilipatikana kiasi shilingi 131.686 bilioni
c. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147; kilipatikana kiasi cha shilingi 510.017 bilioni
d. Sheria ya Ushuru wa Mafuta, SURA, 220; kilipatikana kiasi cha shilingi 155.893bilioni
e. Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, SURA 82 ;kilipatikana kiasi cha shilingi 28.213 bilioni
f. Sheria ya Usalama Barabarani, SURA, 168; kilipatikana kiasi cha shilingi 19.710 bilioni
g. Sheria ya Petroli (Petroleum Act) SURA, 392;kilipatikana kiasi cha shilingi 123.725 bilioni
Hali hiyo ilifanya marekebisho yote ya sheria za Kodi zilizofanywa katika mwaka huo wa fedha kuiwezesha serikali kukusanya jumla ya shilingi 1.018 Trilioni katika mwaka wa Fedha 2013/2014 na hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Hansard ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hali hii haikubaliki na haivumiliki hata kidogo. Hapa tumezungumzia Wizara tatu tu za serikali kuu bado wizara 30 na idara mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na Halmashauri na Taasisi na Mashirika ya Umma.
Ripoti hizi zimezidi kudhihirisha kwa mara nyingine kuwa matatizo yanayowakabili Watanzania ikiwa ni pamoja na umaskini, maradhi, ujinga yanaendelea kudumu kwa sababu watawala wa Serikali ya CCM wameamua yaendelee kuwepo kwa kukumbatia adui wa nne ambaye ni ufisadi.
Ripoti hizo za CAG ambazo zimeanika ufisadi katika maeneo yaliyokaguliwa ikiwemo Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, mashirika ya umma na miradi ya maendeleo, kwa mara nyingine zimedhihirisha wazi kile ambacho CHADEMA kimekuwa kikisema kwa muda mrefu kwamba ufisadi huu unaoendelea kulitafuna taifa na kuwafanya Watanzania wazidi kuwa maskini ni matokeo ya kushindwa kwa sera, mikakati na mipango ya CCM.
Wakati kasi ya ufisadi inaongezeka kutoka mwaka hadi mwaka kwenye Serikali ya Rais Jakaya Kikwete chini ya usimamizi wa CCM, ndivyo serikali hiyo hiyo inaongeza kasi ya kushindwa kusimamia UWAJIBIKAJI ambayo ndiyo moja ya nguzo muhimu katika kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanaonekana katika kuboresha maisha ya wananchi hususan kuweka fursa za kujitafutia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na hatimaye ustawi wa jamii nzima.
Ufisadi huu hauvumiliki tena. Watanzania wasikubali kuendelea kubeba mizigo ya watawala walioshindwa kutekeleza wajibu wao. Hali ya siasa inazingirwa na sintofahamu kubwa. Uchumi unazidi kuyumba. Kijamii, maisha yazidi kuwa magumu na walioko madarakani wamelewa madaraka. Msamiati wa UWAJIBIKAJI haumo vichwani mwao tena.
Ni mwaka wa Watanzania kuamua kuachana na ufisadi huu.
Imetolewa leo Jumatano, 20 Mei, 2015;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano- CHADEMA